Powered By Blogger

Jumapili, Mei 07, 2017

Yanga yatimua vumbi kweli

YANGA jana ilirudi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Prisons mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 59 sawa na Simba, lakini ikiongoza kwa uwiano mzuri wa mabao.
Simba leo inatarajia kucheza na African Lyon kwenye uwanja huohuo wa Taifa, mechi inayotabiriwa kuwa ngumu kwa upande wake. Iliilazimu Yanga kusubiri hadi kipindi cha pili kuandika bao hilo baada ya Prisons kuonekana kujipanga vizuri kwa kipindi chote cha kwanza.
Amisi Tambwe aliwainua vitini mashabiki wa Yanga waliofika uwanjani hapo baada ya kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 71 akiunganisha mpira wa krosi iliyochongwa na Juma Abdul.
Dakika tano baadaye Obrey Chirwa aliwaandikia mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu bao la pili akiunganisha vema pasi ya Geofrey Mwashiuya. Bao hilo lilizidi kuwachanganya Prisons ambao sasa walionekana kurudi nyuma wote kuzuia mabao zaidi baada ya Yanga kuonekana kufunguka zaidi kushambulia.
Kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Toto African imejisogeza mpaka nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo huku ikiishusha JKT Ruvu baada ya kuifunga mabao 2-1. Ruvu sasa inasubiri kumaliza ratiba na kuungana na timu nyingine mbili zitakazofanya jumla ya timu tatu zitakazoshuka daraja kwani sasa hata ikishinda mechi zote zilizosalia haiwezi kupanda.
Katika mechi ya jana, Ruvu ilikuwa ya kwanza kuandika bao la uongozi katika dakika ya kwanza likifungwa kwa shuti kali na Hassan Dilunga ndani ya 18. Toto ilichomoa bao hilo dakika ya 20 kupitia wa Waziri Junior akiunganisha krosi ya Mohamed Soud kabla ya kuunganisha mpira kwa kichwa na kuujaza wavuni.
Junior aliifungia tena Toto bao la pili katika dakika ya 35 akiunganisha pasi ya Jamal Soud. Katika mechi nyingine zilizochezwa jana, Majimaji imeendelea na harakati zake za kupambana kubaki Ligi Kuu baada ya kuifunga Mwadui mabao 3-0 kwenye uwanja wa Majimaji Songea, Ruvu Shooting ikiwa nyumbani Mabatini Mlandizi ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar

Toa maoni yako
Kupitia Facebook.com/proffesa nazir Hamzatz

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni