Powered By Blogger

Jumapili, Mei 07, 2017

DC(mkuu wa wilaya ya Ilala kula sahani moja na wanaokwamisha kodi

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, amesema hatawafumbia macho wenyeviti wa Serikali za Mitaa watakaokuwa kikwazo cha wananchi kulipa kodi za majengo kwa kuwa jambo hilo si la kisiasa.
Aidha, Wenyeviti wa serikali za mitaa katika wilaya hiyo wamekubali mamlaka ya ukusanyaji wa kodi za majengo kukabidhiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwa itasaidia katika kukusanya kiwango sahihi.
Akizungumza wakati wa kufungua semina ya siku moja kwa wenyeviti wa serikali za mitaa, Watendaji wa Kata na mitaa, Mkuu huyo wa wilaya alisema, suala la ukusanyaji wa kodi si jambo la kisiasa bali ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote.
“Sitegemei nyinyi mkawe kikwazo cha wananchi kulipa kodi, nategemea hatatokea mmoja wenu akasimame na kuwa kikwazo. Hatutakubali mtu asimame kati ili kukwamisha wananchi wasilipe kodi, huyo tutamchukulia hatua na katika hili sitataka mchezo,” alisema Mjema.
Akizungumzia semina hiyo, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Manispaa ya Ilala, Ubaya Chuma, alisema wanaamini hatua hiyo kwa sasa itasaidia kwa kuwa yapo mambo ambayo yamerekebishwa.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani, Yusuf Salum Yusuf, alisisitiza kuwa kwa sasa fedha zitakazokuwa zikikusanywa zitaerejeshwa kwa wakati ili mitaa iweze kufanya maendeleo yake.
Alisema kwa mwaka 2015/16 walikuwa na lengo la kukusanya Sh bilioni 7.82 lakini kwa mwaka huu wa fedha 2016/17 lengo lao ni kukusanya Sh bilioni 12.5, ambayo ni ongezeko la asilimia 55.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni