Powered By Blogger

Jumanne, Mei 09, 2017

Operation yaendelea Rwanda kuhusiana na mauaji ya kimbali

WATUHUMIWA nane vinara wa mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda mwaka 1994, bado wanasakwa kwa udi na uvumba na Umoja wa Mataifa ili wajibu tuhuma za ushiriki wao katika mauaji ya watu milioni moja nchini humo wengi wao wakiwa Watutsi.

Kati ya hao nane, watatu ambao ndio watuhumiwa wakuu watashtakiwa katika chombo kinachosimamia kazi zilizobaki za iliyokuwa Mahakama ya Mauaji Kimbari ya Rwanda (ICTR) ambayo imemaliza muda wake miaka miwili iliyopita.

Chombo hicho (MICT) kimepewa majukumu ya kuwatafuta, kuwakamata na kuwashtaki watuhumiwa watatu vinara wa mauaji hayo wakiongozwa na mfanyabiashara Felicien Kabuga ambaye anatajwa kuwa mmoja wa vinara wa mauaji hayo ya siku 100 nchini humo.

Ofisa Habari wa MICT,Danford Mpumillwa alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa kazi ya kuwasaka watuhumiwa hao inaendelea kwa kushirikiana na serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Aliwataja watuhumiwa wengine wawili vinara ambao wakikamatwa watafikishwa katika MICT mjini  Arusha kuwa ni Augustin Bizimana ambaye alikuwa Waziri wa Ulinzi katika serikali ya Rais Juvenal Habyarimana na Protais Mpiranya  aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha kumlinda Rais Habyerimana.

Watuhumiwa wengine watano, kwa mujibu wa Mpumillwa, wakikamatwa watapelekwa Rwanda kushtakiwa ambao ni Fulgence Kayishema, Charles Sikubwabo, Aloys Ndimbati, Pheneas Munyarugarama na mwingine aliyefahamika kwa jina moja tu la Ryandikayo.

“Nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zinawajibika kuwakamata na kuwafikisha katika chombo hicho watuhumiwa hao na kikosi maalum cha kuwasaka kinaendelea kuwafuatilia katika nchi ambazo tunaamini wamejificha. Sasa ni wajibu wa serikali husika kushirikiana kuwakamata watuhumiwa ili wakajibu tuhuma dhidi yao na hii ni kazi ya kudumu,” alisisitiza Mpumillwa wakati wa mkutano wa pamoja wa majaji wa Chombo hicho, Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu (ACPHR), Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) na Mahakama Kuu ya Tanzania.

Akizungumza baada ya ufunguzi wa mkutano huo wa pili kufanyika Afrika, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alisema kuwa una lenga kubadilishana uzoefu katika utoaji wa haki nchini.

“Tunajifunza kutoka kwa wenzetu namna bora na mazingira yatakayosaidia utoaji wa haki hapa nchini kwa kuzingatia uzoefu wa wenzetu na uwezo wa rasilimali walizonazo na hii itasaidia nasi kuiga yale yaliyo ndani ya uwezo wetu,” alisisitiza Profesa Juma.

 MICT ni chombo kilichoundwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya ICTR kumaliza muda wake kusimamia kesi zilizobaki na kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka muhimu za kesi hizo zitakazotumiwa na wasomi kwa ajili ya utafiti wa kitaaluma kikiwa na makao makuu yake Lakilaki eneo la Kisongo jijini hapa.
Au maoni yako Kupitia
NazirHamza au

FacebookTwitterGoogle+WhatsAppPinterestShare

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni