Powered By Blogger

Jumapili, Mei 07, 2017

Kampuni zaalikwa maonesho ya madini

KAMPUNI ya wazawa ya Sky Associated Group ya Arusha inayomiliki mgodi wa TanzaniteOne ni miongoni mwa kampuni pekee iliyojitokeza kuuza madini aina ya tanzanite kwenye Maonesho ya Sita ya Madini.
Mnada huo unafanyika kwa siku tatu katika maonesho hayo kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ambapo mara baada ya ukamilishwaji wa uuzaji wa madini hayo, serikali itapata mapato.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini katika Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe wakati alipozungumza kuhusu uuzaji wa madini hayo kwa mnada kwenye maonesho hayo yaliyoanza jana hadi Mei 5, mwaka huu.
Profesa Mdoe alisema kampuni hiyo ni pekee iliyojitokeza kuuza madini yake katika mnada huo unaofanyika kwenye maonesho hayo, lakini pia wachimbaji wadogo nao wamesisitizwa kutumia fursa hiyo kuyatangaza madini hayo pamoja na kuyauza kwa wafanyabiashara wakubwa wanaohudhuria maonesho hayo kutoka nchi mbalimbali.
“Tulitoa muda kwa kampuni nyingine za madini ya tanzanite kushiriki katika maonesho haya, lakini hazijajitokeza, hivyo Kampuni ya TanzaniteOne ndio itakayouza madini haya katika maonesho haya na natoa rai kwa wachimbaji wadogo kuongeza umahiri zaidi katika kuweka nakshi pamoja na kupata masoko ya ndani na nje ya nchi,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bandera ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maonesho hayo ya vito, alisisitiza kuwa ni vyema sasa serikali ikajenga jengo la Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZ) wilayani Simanjiro ili kuwezesha madini hayo kuuzwa kwa wingi na wageni kutoka nchi mbalimbali kuja kuwekeza nchini.
Dk Bendera alisema madini hayo hayapatikani maeneo mengine, bali Tanzania pekee hivyo ni vyema yakaongezwa thamani ikiwemo kupatikana kwa soko la uhakika ili kila mwananchi ayanunue badala ya wageni kutoka nchi nyingine kuyanunua na kuvaa kama vito.
Awali, akitembelea maonesho hayo, mmoja kati ya washiriki, Osman Abdulsattar kutoka Kampuni ya Gem Tanzanite Ltd, alitoa rai kwa serikali kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye madini ya tanzanite ili Watanzania wanunue na kuvaa kama vito na wengine kutumia kama mapambo kwenye miili yao

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni