WABUNGE wameelezea kushtushwa na msiba wa watoto 33 uliotokea Arusha huku wakitaka kukatwa posho zao kwa ajili ya rambirambi kwa wazazi wa watoto hao. Sambamba na hilo, wameshauri wanafunzi waliopona kwenye gari hiyo wapatiwe tiba ya akili kwa kupewa ushauri nasaha ili wasiathirike kisaikolojia.
Akizungumza na gazeti hili, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema), ameshauri leo Bunge liahirishwe ili kuungana na Watanzania kuomboleza msiba huo wa kitaifa na kufafanua “mbona tunaahirisha Bunge kwa kifo cha mtu mmoja hivyo hawa ni wengi tuahirishe pia.” Aliwashauri wabunge wenzake kukubali kukatwa posho za siku mbili kwa ajili ya kutoa rambirambi kwa wazazi wa watoto hao.
Kwa siku mbunge analipwa Sh 220,000 kama posho ya kikao. “Nilivyosikia taarifa hizi nilipandwa na shinikizo la damu nikashindwa kwenda kwenye mechi kati ya wabunge na Benki ya NMB na nilikuwa mchezaji. Mimi pia ni mama na nina mtoto wa darasa la sita, tuwaombee wazazi wa watoto hao kwani msiba ni mzito sana,” aliongeza Bulaya. Naye Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), ambaye anatokea mkoani Arusha, alitaka Bunge na Taifa kuonesha limeguswa na msiba huo ulitokea kwa shule iliyoongoza kimkoa na kiwilaya mwaka jana kwa kikao cha Bunge leo kusitishwa.
Alitaka serikali kuonesha imeguswa na msiba kwa kushiriki kikamilifu na kuongeza “iliwahi kutokea Arusha watu chini ya ishirini walipoteza maisha kwenye machimbo ya mchanga kwa kuangukiwa na kifusi, aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alikuja msibani, serikali iliwapa fedha wafiwa na ilinunua majeneza.” Mbunge wa Mkinga, Dustan Kitandula (CCM), alisema ni msiba wa kitaifa kwani taifa limeondokewa na nguvu kazi iliyotegemewa kuja kuhudumia taifa. Alishauri kufanyike utafiti nchi nzima wa maeneo maarufu kwa ajali za mara kwa mara ili hatua zichukuliwe na kuokoa maisha ya watu.
“Mtoto aliyebaki kwenye ajali nashauri ahamishwe shule ingawa hilo ni utashi wa mzazi na wengine wote walio kwenye gari nyingine ambao wamepona wafanyiwe tiba ya akili, wapewe ushauri nasaha kwani tukiacha wataathirika hata kwa miaka ya baadaye,” alishauri Kitandula. Mbunge wa Mbinga, Sixtus Mapunda (CCM), mbali na kusikitishwa na kuwataka wazazi wapewe moyo, alisema kwa mazingira ya ajali husika, wote waliokuwapo kwenye basi lile hawakufunga mkanda na hiyo imechangia wengi kupoteza maisha.
“Wangefunga mkanda kwenye ile coaster lazima wengi wasingekufa hasa waliokaa nyuma maana unaona kabisa kule kulikuwa salama, pia madereva sasa wadhibitiwe kudhibiti mwendo,” alieleza Mapunda. Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Mmasi (CCM), aliwataka wamiliki wa shule kuwekeza zaidi kwenye usalama wa wanafunzi kama inavyotumia nguvu nyingi kuwekeza kwenye biashara ya shule kwa kufunga vidhibiti mwendo, ili uongozi wa shule ujue gari linapokwenda na kasi inayokuwa nayo na si kumtegemea dereva kumlinda mtoto. “Ukiangalia ile ajali unaona kabisa gari lilikuwa chakavu, nina shaka na uimara wake, nashauri wenye shule watumie magari yaliyokaguliwa na Sumatra na ubora uangaliwe na TBS,” alieleza Mmasi.
Toa maoni yako Kupitia Facebook.com/proffesa%nazirhamzatz
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni