Powered By Blogger

Ijumaa, Mei 26, 2017

RAMADHANI KAREEM : Waislamu waanza kufunga kesho

Waumini wa dini ya kiislamu kote ulimwenguni wanatarajiwa kuanza kutekeleza ibada ya swaum kuanzia kesho ama kesho kutwa kulingana na kuandama kwa mwezi.
Saum ni nguzo ya nne ya dini ya kiislamu ambapo hujizuia na kula na kunywa hadi jioni pamoja na kutekeleza ibada kwa wingi.
Viongozi wa dini ya kiislamu katika kaunti ya Taita Taveta sasa wanaitaka serikali ya kitaifa kuhakikisha kuna usalama wa kutosha katika maeneo ya ibada na hasa misikiti wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan unapoanza.
Also read:

Mahakama yahahirisha kesi ya kuwaadhibu madaktari wanaogoma

Wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza kuu la waislamu katika kaunti ya Taita Taveta Washallah Abdhi,wanasema mwezi huu ni muhimu kwa kalenda ya jamii ya waislamu na ni sharti usalama uimarishwe kuwezesha jamii hio kutekeleza ibada zao bila matatizo

Jumamosi, Mei 13, 2017

Kuhusu wenye vyeti feki kulipwa mafao


Watumishi waliobainika na vyeti feki, watalazimika kusubiri mafao yao hadi utaratibu wa kuwalipa utakapofanyika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Amina Mollel.

Amina alitaka kujua ni hatua gani zitachukuliwa ili kuwalipa mafao yao wafanyakazi waliobainika na vyeti feki.

Waziri Kairuki alisema, ofisi yake itaandaa utaratibu wa mafao ya wafanyakazi hao na pindi utakapokamilika, watajulishwa na kulipwa haki zao.

Aidha,  Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera , Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu, Anthony Mavunde, alisema kwamba seeikali inaendelea na mchakato wa kuunganisha mifuko ya jamii.

Mavunde alisema hayo alipojibu swali la msingi la Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almas Maige, aliyetaka kujua mchakato wa kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii, umefikia hatua gani.

Mavunde alisema, serikali kwa sasa inafanya tathmini ya mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo imetoa mapendekezo kuhusu namna bora na mambo ya kuzingatiwa katika mchakato wa kuunganisha mifuko hiyo.

Alisema, wadau vikiwemo vyama vya waajiri, vimeshirikishwa ili kutoa maoni na mapendekezo kwa serikali na kutoa maamuzi.

Proffesa J amshangaa Waziri mwakyembe kutaka wasanii wasiimbe siasa

WASIIMBE SIASA

 Saturday, May 13, 2017     burudanisiasa   

Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay, ametoa maoni yake kuhusu ushauri wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyewataka wasanii wa Tanzania kuacha kuimba nyimbo zenye jumbe za kisiasa kwani hawatafanikiwa.

Profesa Jay ambaye ni rapa nguli wa kizazi kipya aliyewahi kuweka rekodi maalum ya albam yake ya ‘Mapinduzi Halisi’ iliyokuwa na jumbe zenye mlengo wa kisiasa na kijamii, amesema ameshangazwa na kauli ya Waziri.

“Kuwaambia wasanii kuwa waimbe nyimbo za maisha yao tu na washindwe kuimba vitu vingine, maana yake unataka kutoa ‘green light’ kwa wasanii sasa waanze kuimba mambo ya mapenzi… nakupenda, nakupenda..,” alisema Profesa Jay.

“Maana yake unaweza kuchochea kuhusu masuala ya mapenzi tu na kushindwa kufanya vitu vya kijamii ambavyo vingeweza kulipeleka taifa letu mbele. Mimi naamini msanii ana sauti kubwa na anaweza kupaza sauti positively na ikasaidia taifa letu ideologically (kiitikadi), socially (kijamii), culturally (kitamaduni), economically (kiuchumi), politically (kisiasa) pamoja na sustainable development (maendeleo endelevu),”aliongeza.

Mbunge huyo alidai kuwa wapo wasanii walioimba kuhusu siasa na masuala ya kijamii kama 2Pac, BIG, Bob Marley, Lucky Dube na wengine ambao walisaidia dunia kuhama katika ngazi moja kijamii hadi ngazi nyingine.

Hata hivyo, Profesa Jay alikubaliana na hoja ya Waziri Mwakyembe kuwa wasanii hawapaswi kuitukana Serikali, akieleza kuwa wanapaswa kuachwa watoe mawazo yao mbadala ikiwa ni pamoja na kuisifia Serikali.

Akizungumza Bungeni mjini Dodoma, Waziri Mwakyembe aliwashauri wasanii kuachana na nyimbo za siasa kwani hawatafanikiwa kwakuwa hakuna msanii ambaye alijikita katika kuimba siasa na akafanikiwa. 

Kuhusu wenye vyeti feki kulipwa mafao


Watumishi waliobainika na vyeti feki, watalazimika kusubiri mafao yao hadi utaratibu wa kuwalipa utakapofanyika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Amina Mollel.

Amina alitaka kujua ni hatua gani zitachukuliwa ili kuwalipa mafao yao wafanyakazi waliobainika na vyeti feki.

Waziri Kairuki alisema, ofisi yake itaandaa utaratibu wa mafao ya wafanyakazi hao na pindi utakapokamilika, watajulishwa na kulipwa haki zao.

Aidha,  Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera , Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu, Anthony Mavunde, alisema kwamba seeikali inaendelea na mchakato wa kuunganisha mifuko ya jamii.

Mavunde alisema hayo alipojibu swali la msingi la Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almas Maige, aliyetaka kujua mchakato wa kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii, umefikia hatua gani.

Mavunde alisema, serikali kwa sasa inafanya tathmini ya mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo imetoa mapendekezo kuhusu namna bora na mambo ya kuzingatiwa katika mchakato wa kuunganisha mifuko hiyo.

Alisema, wadau vikiwemo vyama vya waajiri, vimeshirikishwa ili kutoa maoni na mapendekezo kwa serikali na kutoa maamuzi.

Wabunge wahuzunika sana kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha

Wakazi wa Videte Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani wakivuka mto Mzinga kwenda Bamia karibu na Uwanja wa Azam Complex Chamazi Manispaa ya Temeke Dar es Salaam. Wakazi hao wameomba kusaidiwa daraja kwa kuwa uvushaji huo ni hatari kwa maisha yao hasa kipindi hiki cha mvua. Wakazi hao wanavushwa kwa shilingi 1000 kwa kila kichwa.

0 Comments

ATHARI za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko na maporomoko katika sehemu mbalimbali nchini jana ziliwagusa wabunge na kutaka Bunge liahirishe shughuli zake ili wabunge waijadili hali hiyo iliyoathiri miumdobinu, makazi na hata kusababisha vifo.

Mvua hizo zinazoendelea kunyesha kwa takribani wiki tatu mfululizo sasa, zimeacha athari kubwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Zanzibar. Wabunge walioomba mwongozo baada ya kumalizika Kipindi cha Maswali na Majibu ni Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), Mbunge wa Vunjo James Mbatia (NCCR Mageuzi) na wa Mlalo, Rashid Shangazi (CCM).

Ngonyani maarufu kama Profesa Majimarefu alisema kuna matatizo makubwa ya mafuriko nchini. “Kwenye mkoa wangu wa Tanga kumekuwa na maafa, leo (jana) hii kuna watu 1,000 hawana chakula, mahali pa kuishi na hawana msaada wowote, lakini serikali itawasaidiaje hawa watu wakati kamati za afya zikiendelea na utaratibu,”alisema. Kwa upande wa Shangazi alitaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili wabunge wajadili kuhusu mafuriko hayo.

“Sasa hivi katika mkoa wa Tanga kuna mafuriko makubwa sana. Jana (juzi) yametokea maporomoko katika milima ya Usambara, eneo la barabara za Lushoto- Arusha- Mombo , Pangani kwenda Tanga, Mombo kwenda Lushoto na Kilindi kwenda Morogoro zote zilifungwa,”alisema.

Alisema Mkoa wa Tanga umegeuka kuwa kisiwa umepata athari kubwa hasa Korogwe na kuiomba Serikali ilione hilo jambo ni la kimkakati na kwamba Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) amezidiwa .

Alisema barabara hizo zimekuwa zikiunganisha mkoa huo na mikoa mingine na kutaka Bunge lijadili angalau kwa muda mfupi. Naye Mbatia alisema hali ni tete kutokana na mafuriko yaliyojitokeza na kuomba utu wa mwanadamu kuzingatiwa kama wawakilishi wa Watanzania kwa kutenga muda wa angalau dakika 15 kujadili suala hilo.

“Tutenge muda wa dakika 15 ama 20 ili tujadili suala hili, ambayo ni ya maafa tunaweza tukatoa majibu sahihi kwa wapiga kura wetu, mwenyekitindio ombi langu kwa mujibu wa kanuni nilizozitumia,”alisema.

Akijibu miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisema miongozo ya Mbatia na Shangazi imeangukia katika kanuni ya 47 (1) ambayo inasomwa pamoja na kanuni ya 48. “Lakini kanuni ya 47(4) inampa Spika mamlaka aridhike kama ombi hilo anaona jambo hilo kweli linahitaji kusitisha shughuli zilizo mbele yetu ili kujadili hoja hizo za dharura,”alisema.

Hata hivyo, alisema kwa hali anayoiona haoni kama suala hilo linahitaji kujadiliwa sasa. “Ni kweli tukio hili limegusa maeneo mengi, nawapa pole walioguswa kwa namna moja hata nyingine. Naamini Serikali iliyoko humu ndani itaitolea maelezo wakiangalia nchi nzima,”alisema na kuongeza kuwa, anaamini Serikali italizungumzia vizuri kuliko kila mbunge kujisemea katika eneo lake.

Kuhusu mwongozo wa Ngonyani, Chenge alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 68 (7) ni lazima liwe tukio ama jambo ambalo limetokea mapema bungeni na si nje. Polisi asombwa, afa Wakati wabunge wakitaka kujadiliwa kwa athari za mvua zinazoendelea kunyesha, askari wa Jeshi la Polisi, Abbas Anas Haji (55) amekufa maji baada ya kusombwa akiwa na pikipiki yake aina ya Vespa wakati akipita eneo la barabara ya Fuoni Kibondemzungu lililofunikwa na maji. Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 5:30 asubuhi wakati askari huyo akitokea kazini kwenda nyumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Hassan Nassir Ali alisema marehemu alikuwa ni mfanyakazi wa jeshi la polisi katika Kitengo cha Picha, Makao Makuu ya Polisi upande wa Zanzibar.

Familia 150 zatangatanga Katika tukio jingine, zaidi ya familia 150 kisiwani Pemba zimekosa makazi na kulazimika kusitiriwa na ndugu na jamaa baada ya nyumba zao kuathirika vibaya na mvua kubwa iliyonyesha kwa siku tatu mfululizo.

Timu ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyotembelea mikoa miwili Pemba na kujionea athari za mafuriko, imeelezea kufurahishwa na mshikamano mkubwa uliooneshwa na wananchi katika kusaidiana bila ya kujali itikadi za kisiasa.

Waziri asiye na Wizara Maalumu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Juma Khatib alisema wananchi wameonesha uzalendo wa hali ya juu ambao watu wote walioathirika na mafuriko hayo wamehifadhiwa na kuishi kwa ndugu na jamaa.

Aidha, Khatib waliwataka wananchi walioathirika na mafuriko hayo wasirudi tena katika maeneo yao hayo ambayo athari zake bado zipo. Ameahidi kusaidia na kutoa mifuko ya saruji 50 kwa familia za wilaya ya Mkoani ili zikarabati nyumba zao.

Tanga-Arusha yafunguka Aidha, mkoani Tanga ambako miundombinu ya barabara ilisababisha kukusekana kwa usafiri kati ya mkoa wa Tanga na mikoa jirani ya Kilimanjaro na Arusha, hali imetajwa kurejea katika hali yake ya kawaida.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel akizungumza jana katika mahojiano kwa njia ya simu alisema kiasi cha mvua inayonyesha kimeanza kupungua ingawa ipo hali ya mawingu mazito katika baadhi ya maeneo.

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba akizungumzia hali ya usalama kuhusu kifusi kilichoanguka na kufunga sehemu ya eneo la barabara kuu inayounganisha miji ya Soni na Lushoto alisema anaelekea eneo la tukio na kwamba atatoa taarifa.

Aidha, kuhusu mawasiliano ya barabara ya Tanga - Pangani alisema kwa sasa watumiaji wa barabara hiyo wanapita katika njia mbili mbadala ikiwemo ya Pongwe - Kirare jijini Tanga pamoja na ile ya Muheza- Misozwe - Pangani ya wilayani Muheza wakati huu ambapo Tanroads wanafanya jitihada za kutengeneza njia ya mchepuko katika eneo la daraja la Neema lililopo kwenye barabara kuu ya Tanga- Pangani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa ameuagiza uongozi wa Jiji la Tanga kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wajitahidi kufanya utafiti wa maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja nyakati za msimu wa mvua badala ya kiangazi ili kupata picha ya mahitaji halisi ya ujenzi tofauti na inavyofanyika sasa.

Ametoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti jana alipozungumza katika mahojiano na HabariLeo baada ya kutembelea baadhi ya mitaa ya jijini Tanga iliyoathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua isiyo ya kawaida iliyonyesha mfululizo juzi kwa saa 24 na kusababisha maafa ikiwemo vifo vya wakazi wawili.

Katika mji wa Tanga, mvua hizo ziliua watu wawili, nyumba 97 zilizingirwa maji pamoja na Soko maarufu la vyakula la Magandini na kusababisha mali zote kupotea, nyingine 36 zilibomoka kabisa, moja kutitia, nyingine kuteketea kwa ajali ya moto uliotokana na hitilafu ya umeme ambapo kaya 59 zenye wakazi zaidi ya 200 walioathirika walihifadhiwa katika kambi zilizopo kwenye shule ya msingi ya Chumbageni, Kwakaheza, Magaoni, Mafuriko na Sekondari ya Hotten.

Mvua za kihistoria Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) hivi karibuni ilitoa taarifa inayoonesha kuwa, mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali mkoani Tanga zimefikia kiwango cha juu ambacho hakikuwahi kurekodiwa tangu mwaka 1949, sawa na takribani miaka 68 iliyopita.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Utafiti wa mamlaka hiyo, Dk Ladislauds Chang’a, mvua iliyonyesha kwa saa 24 Mei 9 mwaka huu mkoani Tanga ni ya milimita 316, kiwango ambacho hakijarekodiwa kwa miaka mingi.

Aliongeza kuwa, hawajafanya tathimini, lakini mwaka 2014 kulikuwa na kiwango kikubwa zaidi baada ya kunyesha mvua ya milimita 138 ndani ya saa 24 na kwamba kiwango cha juu kwa historia ya kituo cha Dar es Salaam ni mwaka 1953 iliponyesha mvua ya kiwango cha milimita 167.4. Alisema mvua za sasa zinatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi huu.

Ijumaa, Mei 12, 2017

Watumishi wawili wa Serikali Mwambungu & Sozigwa waaga dunia

Mwambungu, Sozigwa wafariki dunia

IMEANDIKWA NA WAANDISHI WETUIMECHAPISHWA: 13 MAI 2017

 Kuchapa   Barua pepe

0 Comments

TAIFA limepata pigo la kuondokewa na watumishi wa Serikali wa muda mrefu, mwanahabari nguli aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kwanza wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, Paul Sozigwa na aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu.

Wawili hao walifikwa na mauti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) walikokuwa wamelazwa kwa matibabu. Sozigwa ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Kwanza wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD, sasa TBC baada ya kuwa Shirika la Utangazaji Tanzania), alifikwa na mauti jana saa nane usiku wa kuamkia jana kutokana na matatizo ya moyo , wakati Mwambungu pia aliaga dunia jana asubuhi kutokana na maradhi ya figo.

Msemaji wa JKCI, Anna Nkinda alithibitisha kutokea kwa vifo vya Mzee (84) aliyekuwa amelazwa tangu Aprili 25, mwaka huu akitokea Wodi ya Mwaisela ya Hospitali ya taifa Muhimbili (MNH) na Mwambungu (62) ambaye alifikishwa hospitalini hapo Mei 10 mwaka huu saa nane mchana.

Mtoto wa kwanza wa marehemu, Hamidu Mwambungu alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa na tatizo la figo kwa zaidi ya mwaka mmoja na ni ugonjwa ambao umemsababishia mauti hayo.

Alisema familia inaendelea kupanga taratibu za maziko. “Hatujajua mazishi yatafanyika lini na wapi bado wanafamilia tunakutana kupanga lakini nadhani tunaweza kuzika mwishoni mwa wiki hii,” alisema Hamidu. Hamidu alisema msiba huo uko nyumbani kwa marehemu Tabata Kimanga, Dar es Salaam.

Mzee Sozigwa “Mzee Sozigwa alikuwa akisumbuliwa magonjwa mengine pia, aliletwa hapa akiwa na tatizo la moyo, akatibiwa hapa akawa amepona lakini alibaki hapa wakati akiendelea na matibabu ya yale magonjwa mengine mpaka leo (jana) alipofariki,” alisema Nkinda.

Mtoto wa marehemu, Mchungaji wa Kanisa la KKKT, Moses Sozigwa alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo, matatizo ya tumbo, na pia shida mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupoteza kumbukumbu inayotokana na kuwa na umri mkubwa.

Aidha, alisema familia inaendelea kupanga mazishi ya baba yao na kwamba msiba huo uko nyumbani kwake Mtoni Mtongani, Temeke kwenye Kanisa la KKKT ambako ni maarufu kama maskani ya Kwaya ya Lulu.

Mbali ya kuwa Mkurugenzi wa RTD na baadaye mwaka 1967 kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais, Sozigwa alikuwa kada mzuri wa chama tawala, CCM alikokuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Pwani, lakini pia akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho. Sozigwa atakumbukwa kutokana na weledi na uadilifu wake katika kutimiza majukumu yake.

CCM kimetoa salamu za rambirambi kwa msiba huo wa Sozigwa ambapo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amesema kuwa chama kimepokea kwa masikitiko taarifa za msiba huo. “Mzee Sonzigwa alihudumia na kutoa huduma kwa utumishi uliotukuka ndani ya chama na pia serikali kabla na baada ya uhuru na pia alihudumia kama katibu wa kwanza wa Rais Mwalimu Nyerere,” alisema Polepole.

Alisema chama hicho kitamkumbuka na kumuenzi na jambo ambalo alishughulika nalo ni pamoja na kushughulikia misingi na maadili na miiko ya uongozi ndani ya CCM. Naye Naibu Katibu Mkuu CCM (Bara),Rodrick Mpogolo, amemtaja Mwambungu kuwa alikuwa kiongozi mwadilifu katika utendaji wake wa kazi ndani ya CCM alipokuwa Mkuu wa Utawala Makao Makuu (Ofisi Ndogo) Lumumba, Dar es Salaam na hata alipoteuliwa kuwa mtumishi wa Serikali.

“Tumempoteza kiongozi mahiri na shupavu … watu wanakumbukwa kwa yale mazuri unayofanya hapa duniani na Mwambungu atakumbukwa kwa mema aliyoyetenda wakati wa uhai wake,” alisema Mpogolo akiwa mjini hapa.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) mkoa wa Morogoro, Christine Ishengoma, alisema alimfahamu Mwambungu wakati yeye (Dk Ishengoma) alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani mwaka 2006 na aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

“Nimeshistushwa na kifo chake …ninaweza kusema kuwa Mwambungu ndiye aliyenipokea wakati nikiwa mkuu wa mkoa wa Pwani na yeye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha na makao makuu ya mkoa ni Kibaha,” alisema Dk Ishengoma.

Pamoja na hayo alisema kuwa, mara baada ya Mwambungu kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa na kupangiwa mkoa wa Ruvuma, Dk Ishengoma alisema alimpokea na kukabidhi mkoa huo wakati yeye akihamishiwa mkoa wa Iringa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe, alimtaja Mwambungu kuwa licha ya kumfahamu kupitia vyombo vya habari, alifahamiana yake wakati walipoteuliwa kuwa wakuu wa mikoa.

“Mwambungu alikuwa mcheshi, alikuwa karibu na wananchi na pia ni mpenda utani ni hazina kuu imepotea, lakini ni mapenzi ya Mungu,” alisema. Baadhi ya viongozi wa CCM, wakiongozwa na Mwenyekiti wao mkoa wa Morogoro, Innocent Kalogeries na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro mjini kichama, Fikiri Juma kwa nyakati tofauti waliwajulisha wajumbe walioshiriki kikao hicho juu ya kutokea kwa msiba huo.

Momogoro blog ;watendaji wa shule ya Lucky Vincent wapandishwa kizimbani

WAKATI Mkurugenzi wa Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vincent ya jijini Arusha, Innocent Mushi na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Longino Nkana wakipandishwa kizimbani kutokana na vifo vya watu 35 wakiwemo wanafunzi 32 wa shule hiyo, ndege maalumu inatarajiwa kutua nchini leo kuwabeba majeruhi watatu wakatibiwe Marekani.

Mwinjilisti maarufu duniani kutoka Shirika la Samaritan Purse, Bill Graham wa Marekani na ndiye aliyebeba gharama za kukodisha ndege maalumu aina ya DC 8 kupeleka wanafunzi waliojeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani Karatu, Arusha.

Watoto hao wameumia shingo, miguu na sehemu mbalimbali za miili yao. Kwa mujibu wa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyarandu aliyezungumza jana na waandishi wa habari mjini Arusha, gharama za kukodisha ndege kwenda Marekani si chini ya dola za Kimarekani 350,000 (Sh milioni 700). Gharama hizo ni nje ya matibabu, chakula na malazi kwa wakati wote ambao wagonjwa hao na wasindikizaji watakuwa nchini humo.

“Tumefanikiwa kupata ndege aina ya DC 8 kutoka Shirika la Samaritan Purse linaloongozwa na mtoto wa Billy Graham aitwaye Franklin kwa ajili ya kuwasafirisha watoto Doreen Mshana, Sadia Awadh na Wilson Tarimo na wazazi wao watatu, yaani mama zao,” alisema Nyalandu akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Alisema pia watoto hao wataambatana na daktari wa hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Elias Mashalla na muuguzi Simphorosa Silalye. Kwa mujibu wa Nyalandu, ndege hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro KIA) leo jioni ikitokea Charlotte ,Jimbo la North Carolina, Marekani.

“Endapo taratibu za safari ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa visa utafanikiwa, basi ndege inaondoka na wagfonjwa na wasindikizaji Jumapili (kesho) na baada ya kufika mjini Charlotte, North Carolina watasafiri kwa ndege nyingine maalumu ya kubeba wagonjwa hadi mji wa Sioux City, Iowa ambako watapokelewa na uongozi wa Hospitali ya Mercu na Shirika la STEMM,” alisema Nyalandu.

Alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kupongeza juhudi za Rais, Dk John Magufuli, Makamu wake, Samia Suluhu Hassan na uongozi wa Mkoa wa Arusha chini ya Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo kwa kuguswa na kushiriki katika kila hatua kuanzia baada ya ajali, mazishi hadi ufuatiliaji wa afya za majeruhi.

‘’Hili jambo ni letu sote hapa, hatuhitaji sifa bali tunachopaswa Watanzania wote kushirikiana kwa pamoja na kuweka mbele ubinadamu na kujitoa kwa hali na mali kuwasaidia hawa watoto ili waweze kupata nafuu na kurudi shuleni,” alisema Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo alisema kuwa katika michango yote iliyochangwa kwa ajili ya rambirambi kwa msiba huo mpaka jana zilipatikana fedha kiasi cha Sh milioni 215.

Gambo alisema katika fedha hizo, kila familia ilikabidhiwa zaidi ya Sh milioni 3.8 na pia Serikali ilibeba gharama za usafiri, majeneza, mafuta ya magari na malipo ya madereva. Alisema Sh milioni 190 zilitumika katika matumizi mbalimbali ya msiba huo na kuwataka walioahidi kuchangia kutimiza ahadi zao.

Kizimbani Wakati majeruhi ambao ni wanafunzi wa shule hiyo wakitarajiwa kupelekwa Marekani, mmiliki wa shule hiyo na mwalimu mkuu msaidizi walipandishwa kizimbani kwa makosa kadhaa ya usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na kusafirisha watoto bila ya kuwa na vibali.

Wakisomewa mashitaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Hakimu Mkazi Arusha, Desdery Kamugisha, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Rose Sule alidai watuhumiwa hao wawili wamefunguliwa kesi Namba 78/2017 huku Mkurugenzi wa shule hiyo akishitakiwa kwa makosa manne na Mwalimu Nkana akishitakiwa kwa kosa moja.

Akimsomea Mkurugenzi wa Lucky Vincent makosa yake, wakili huyo alidai kosa la kwanza ni la kuendesha gari la abiria bila ya kuwa na leseni ya usafirishaji ambapo Mei 6 mwaka huu katika eneo la Kwamrombo, Arusha Mjini akiwa mmiliki wa gari namba T 871 BYS aina ya Toyota Rosa, alifanya shughuli ya usafirishaji bila ya kuwa na leseni ya abiria.

Kosa la pili ni kuruhusu kuendesha gari bila ya kuwa na bima (Road Licence), Mei 6 mwaka huu akiwa mmiliki wa gari hilo aliruhusu gari hilo kuendeshwa bila ya kuwa na bima. Kosa la tatu ni kushindwa kuingia mkataba na mwajiriwa wake, Dismas Gasper ambapo Mei 6, 2017 akiwa mmiliki wa gari alishindwa kuingia mkataba na dereva huyo aliyeendesha gari lililopata ajali ambaye naye alifariki dunia katika tukio hilo.

Kosa la nne ni kubeba abiria zaidi ya 13 ambapo Mei 6 mwaka huu, mkurugenzi huyo ambaye ni Ofisa Msafirishaji na mmiliki wa shule ya Lucky Vincent alibeba na kusafirisha abiria zaidi ya 13 katika gari hilo kitendo ambacho ni kinyume na sheria.

Kosa la tano ni la Mwalimu Mkuu Msaidizi ambapo anashitakiwa kwa kuandaa safari iliyozidi abiria 13 ambapo ni kinyume cha sheria inadaiwa kuwa Mei 6 mwaka huu, Nkana akiwa Mwalimu Mkuu Msaidizi na mwandaaji wa safari alipakia abiria zaidi ya 13 kwenye gari lililosababisha vifo vya wanafunzi hao.

Baada ya washitakiwa hao kusomewa mashitaka yao yanayowakabili wakili anayewatetea washitakiwa hao, Method Komomogolo aliomba dhamana kwa washitakiwa hao huku Wakili wa Serikali Sule akisema hana pingamizi na dhamana yao.

Hakimu Kamugisha alitoa masharti ya dhamana kwa washitakiwa hao ambayo ni kila mshitakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 15 na kwamba hawatakiwi kuondoka nchini au ndani ya mkoa bila ruhusa ya mahakama pamoja na kuwasilisha hati zao za kusafiria.

Watuhumiwa hao walitimiza masharti ya dhamana yao na kesi yao kuahirishwa hadi Juni 8, mwaka huu.